Latest in Tech

IFAHAMU VEMA SAYARI YA DUNIA




Dunia (kutoka neno la Kiarabu; wakati mwingine pia: ardhi na kwa neno asili la Kibantu nchi) ni gimba la angani tunapoishi.
Ni mojawapo ya sayari zinazoelea katika anga ya ulimwengu. Kuna sayari nane zinazolizunguka jua, dunia yetu ikiwa sayari ya tatu katika mfumo wa jua na sayari zake.
Masafa baina yake na jua ni kilomita milioni 150 au kizio astronomia 1. Dunia huchukua siku 365.256 kulizunguka jua, na masaa 23.9345 kuuzunguka mhimili wake na upana wake ni kilomita 12,756.
Dunia huwa na mwezi 1.
Umri wa dunia hukadiriwa kuwa miaka bilioni 4.5[1][2].
Ni mahali pekee katika ulimwengu panapojulikana kuna uhai ulioaminiwa kuanza miaka bilioni 3.5 iliyopita[3].
Uhai unapatikana kwa spishi milioni 10-14 za viumbe hai pamoja na wanadamu waliokadiriwa kuwa sasa bilioni 7.2[4].

Umbo la dunia

Umbo la dunia linafanana na tufe au mpira unaozunguka kwenye mhimili wake. "Mhimili wa dunia" ni mstari kati ya ncha zake.
Lakini si tufe kamili. Ina uvimbe kidogo kwenye sehemu ya ikweta; ilhali umbali kati ya ncha mbili ni kilomita 12,713 lakini umbali kati ya sehemu za kinyume kwenye ikweta ni km 12,756, yaani kipenyo hiki kinazidi takriban kilomita 43 kipenyo kati ya ncha na ncha. Tofauti hii inasababishwa na mzunguko wa dunia. Kani nje inasukuma sehemu za ikweta nje zaidi. Kwa hiyo mahali duniani palipo karibu zaidi na anga la nje si Mlima Everest kwenye Himalaya bali mlima Chimborazo nchini Ekuador.[5]

Nusutufe ya dunia yenye maji mengi
Kwenye uso wake dunia huwa na tofauti kati ya nusutufe zake mbili. Nusu moja ina eneo kubwa la mabara yaani nchi kavu ambayo ni asilimia 47 ya sehemu hii. Kinyume nusutufe nyingine inafunikwa na maji ya bahari na eneo la nchi kavu ni asilimia 11 pekee za maeneo yake.
Kwa jumla dunia ni sayari pekee katika mfumo wa jua yenye maji katika hali ya kiowevu usoni mwake. Bahari kuu ya dunia inashika asilimia 96.5 ya maji yote yaliyopo duniani. Maji ya bahari huwa na asilimia 3.5 chumvi ndani yake.
Kwa pamoja maeneo ya maji hufunika 70.7% za uso wa dunia. Nchi kavu huwa na 29.3% na sehemu kubwa ya eneo la nchi kavu ni bara 7 za Asia, Afrika, Amerika Kaskazini, Amerika Kusini, Antarktika, Ulaya na Australia. (Ulaya inaweza kuangaliwa pia kama sehemu ya Asia ikiwa kama rasi yake ya magharibi. Azimio la kutazama Australia kama bara na Greenland kama kisiwa tu ni azimio la hiari si la lazima).
Maeneo ya bahari kuu ya dunia kwa kawaida hugawiwa kwa bahari kubwa 3 za Pasifiki, Atlantiki na Bahari Hindi. Sehemu ya chini baharini iko kwenye Mfereji wa Mariana katika Pasifiki (mita 11,034 chini ya UB). Kwa wastani bahari huwa na kina cha mita 3,800.

Muundo wa dunia

- taz. makala "Muundo wa dunia" -

Matabaka yaliyopo katika muundo wa dunia.
Tumeona dunia ina umbo la mviringo au tufe. Tufe hilo si kipande kimoja kikubwa cha mwamba thabiti. Dunia ina muundo ndani yake. Muundo huo unafanana kiasi na kitunguu, yaani dunia yetu imefanyika kwa matabaka mbalimbali yanayofuatana kutoka nje kwenda ndani. Kila moja lina tabia yake.
Kimsingi wataalamu hutofautisha matabaka matatu ambayo ni:
Ganda la dunia ni sehemu imara na uhai wote tunaoujua unapatikana juu yake. Katikati hali ya koti na ya kiini ni ya joto kubwa sana na maada yake hupatikana katika hali ya giligili (si imara, kuyeyushwa). Kila ukiingia ndani dunia inazidi kuwa ya moto mpaka ukifika ndani kabisa daraja ya harara hufikia nyuzi 5000-6000 °C.
Matabaka hayo yanafanywa kwa elementi za kikemia ambazo ni feri (chuma) (32,1 %), oksijeni (30,1 %), silisi (15,1 %), magnesi (13,9 %), sulfuri (2,9 %), nikeli (1,8 %), kalsi (1,5 %) na alumini (1,4 %). Mabaki ya 1,2 % ni viwango vidogo vya elementi nyingine. Elementi hizo zinapatikana kwa hali safi au katika kampaundi za elementi.
Vipimo vimeonyesha ya kwamba matabaka mawili ya koti na kiini huwa tena na mgawanyiko ndani yake, hivyo matabaka yafuatayo yanaweza kutofautishwa.
Tabaka Kuanzia kilomita
Ganda la nje 0 - 40
Koti la juu 40 - 400
Koti la kati 400 - 900
Koti la chini 650 - 2900
Kiini cha nje 2900 - 5100
Kiini cha ndani 5100-6371
Sehemu ya juu ya koti inafanana kikemia na ganda na sehemu hizo mbili zinaitwa tabakamwamba. Tabakamwamba ina unene wa kilomita 50 - 100.
Tabakamwamba imekatika katika vipande vinavyoitwa mabamba la gandunia. Vipande hivi vinaelea juu ya giligili ya koti la ndani. Ndiyo sababu bara lolote si la milele; kila bamba huwa na mwendo wake na ndiyo sababu katika historia ya dunia mabara yameachana na kuungana mara kadhaa. Kwa mfano imepimwa ya kwamba sehemu kubwa ya Afrika ya Mashariki ina mwendo wa kuachana na bara la Afrika na dalili yake ni bonde la ufa.
Pale ambako mabamba yanapakana, volkeno nyingi zinapatikana na matetemeko ya ardhi hutokea.

Uga sumaku wa dunia


Mnururisho unavyotoka kwenye jua na kukengeushwa na mistari ya nguvu ya sumaku ya uga sumaku wa dunia
Dunia inazungukwa na uga sumaku yaani mistari ya nguvu ya kisumaku. Sababu yake ni kwamba kiini cha dunia kinafanywa na chuma chenye tabia kama sumaku kubwa.
Tabia hiyo inasababishwa na mwendo wa mikondo ya chuma cha moto kilichoyeyuka katika kiini cha nje cha dunia. Mistari ya nguvu ya sumaku inatoka nje kwenye ncha ya kusini na kurudi ndani ya dunia kwenye ncha ya kaskazini. Tabia hiyo ni msingi wa kazi ya dira ambamo sindano ya dira huvutwa daima na ncha sumaku ya dunia na kuelekea kaskazini muda wote.
Uga sumaku wa dunia ni kinga muhimu kwa uhai wote duniani. Dunia inapigwa muda wote na mnururisho kutoka jua kwa njia ya "upepo wa jua". Mnururisho huo ni nuru pamoja miale ya hatari. Uga sumaku unakengeusha sehemu kubwa ya mnururisho hatari hadi unapita kando ya dunia na kutofika kwenye uso wa dunia.

Share this:

Post a Comment

 
Copyright © bakinamimi. Designed by OddThemes & VineThemes